Okoa Mombasa yatangaza upya mahitaji ya kongamano la umma la kubadilisha jina la bustani la “Mama Ngina Park”

Oktoba 19, 2022

Okoa Mombasa imerejelea matakwa yake kwamba Bunge la Kaunti lifanye kikao cha hadhara kuhusu kubadilisha jina la bustani la “Mama Ngina Park.”

Awali Okoa Mombasa iliwasilisha ombi kuhusu suala hilo mnamo Novemba 2019, mara tu baada ya bustani hiyo mpya iliyokarabatiwa kufunguliwa tena. Bunge la Kaunti lilikubali kuandaa kongamano la umma kujadili suala hilo mnamo Machi 4, 2020 katika Jumba la Kijamii la Tononoka. Kwa bahati mbaya, kikao kilighairiwa kwa njia ya sitofahamu katika dakika ya mwisho – asubuhi ya tukio. Janga la Covid-19 kisha liliikumba Kenya, na suala hilo bado halijashughulikiwa tena.

Ombi jipya lililowasilishwa leo linadai kongamano la umma ambalo limecheleweshwa kwa muda mrefu hatimaye lifanyike.

“Majina ya mahala na sehemu za umma ni muhimu ziwe na sura au majina zinazo ashiria tamaduni na historia za walioishi sehemu hio. Lakini Mama Ngina Park ya Mombasa ni ya kipekee; jina lake halina uhusiano na Mombasa, Pwani au watu wa eneo hilo,” ombi hilo lilisema.

Okoa Mombasa inaamini kuwa jina lililochaguliwa linafaa kuashiria urithi wa kihistoria na tamaduni za watu wa Mombasa, haswa Pwani kwa jumla. Tunataka jina jipya lichaguliwe kupitia mchakato wa uwazi na ushirikishwaji wa umma.

“Leo, tunafufua rasmi ombi letu la 2019, na kutoa nafasi kwa Bunge la Kaunti ya Mombasa kutafuta maelewano na wananchi kuhusu suala hili muhimu,” alisema mwanachama wa Okoa Mombasa Khelef Khalifa. “Hii ni muhimu katika kulinda ugatuzi, ambao tunatazamia kuwapa wenyeji uwezo zaidi wa kuamua juu ya udhibiti na matumizi ya rasilimali ndani ya mamlaka yao. Tunalitaka Bunge liitishe jukwaa la hadhara kuhusu suala hilo haraka iwezekanavyo.”

Katika kura ya maoni isiyo rasmi ya mtandao wa kijamii ambayo Okoa Mombasa aliifanya 2020, Mekatilili Wa Menza Park ilichaguliwa na wapiga kura kama jina kuu, kwa 44.3% ya kura. Mombasa Waterfront Park ilishika nafasi ya pili kwa 32.9% ya kura. Light House Drive Park (16.4%) na Mombasa Port view Park (6.4%) zilikuja katika nafasi ya tatu na ya nne, mtawalia. Okoa Mombasa hauchukui msimamo au haigemei jina lolote isipokua inatumaini kuona jina ambalo itaashiria historia ya pwani.

Kabla ya uchaguzi huo, Okoa Mombasa ilizindua Ahadi yake ya Uchaguzi wa 2022, ambayo iliwataka wagombeaji kuahidi masuala manne muhimu ili kuimarisha Mombasa na Pwani. Ahadi ilitaja kwa uwazi “kushiriki katika zoezi la kuipa jina upya bustani hilo katika Kaunti ya Mombasa.” Jumla ya wagombea tisa walitia saini ahadi hiyo, wakiwemo washindi wa mwisho wa uchaguzi Abdulswamad Shariff Nassir (Gavana) na Seneta Mohamed Faki (Seneta).

Ombi kamili linaweza kusomwa hapa.

Share This